Discover millions of ebooks, audiobooks, and so much more with a free trial

Only $11.99/month after trial. Cancel anytime.

Mbaraka Mwinshehe na Muziki wa Rumba Tanzania
Mbaraka Mwinshehe na Muziki wa Rumba Tanzania
Mbaraka Mwinshehe na Muziki wa Rumba Tanzania
Ebook161 pages1 hour

Mbaraka Mwinshehe na Muziki wa Rumba Tanzania

Rating: 0 out of 5 stars

()

Read preview

About this ebook

Mbaraka Mwinshehe Mwaruka ni moja ya wanamuziki nyota kuwahi kutokea Tanzania. Mwanamuziki huyu alikuwa na kipaji kikubwa cha kupiga gitaa la solo, ala zingine, kutunga na kuimba. Kutokana na utunzi wake wa nyimbo za kusisimua, alijizolea wapenzi wengi wa muziki Afrika Mashariki na ya kati, akipiga zaidi muziki wa mtindo wa rumba, mtindo ambao asili yake ni kutoka Cuba na nchi zingine za Marekani ya kusini. Katika uhai wake, alishiriki kupiga muziki katika bendi za Morogoro jazz na Super Volcano zote za mjini Morogoro. Kitabu hiki Kinaanza kwa kuelezea kuingia kwa muziki wa rumba toka Cuba wakati huo Tanganyika na kuenea kwake, kinajikita zaidi kuelezea mchango wa mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe Mwaruka, katika kuundeleza na kuimarisha muziki huu wa rumba, kama sehemu ya juhudi za kuinua utamaduni wa taifa jipya la Tanzania na changamoto alizopitia.

LanguageKiswahili
PublisherMarwa
Release dateDec 22, 2023
ISBN9798223838692
Mbaraka Mwinshehe na Muziki wa Rumba Tanzania

Related to Mbaraka Mwinshehe na Muziki wa Rumba Tanzania

Related ebooks

Reviews for Mbaraka Mwinshehe na Muziki wa Rumba Tanzania

Rating: 0 out of 5 stars
0 ratings

0 ratings0 reviews

What did you think?

Tap to rate

Review must be at least 10 words

    Book preview

    Mbaraka Mwinshehe na Muziki wa Rumba Tanzania - Marwa

    ANTHONY MARWA MWITA

    Hakimiliki © 2023 Anthony Marwa Mwita

    All rights reserved.

    TABARUKU

    Natabaruku kitabu hiki kwa wazazi wangu Marwa Mwita Taragwa na Chausiku Werema walionilea kwa mapenzi makubwa. Pia kwa mke wangu mpendwa Mbilijao Philipo na wanangu Wilbrod Anthony, Taragwa Anthony, Sophia Anthony na Mossi Ramadhan

    .

    YALIYOMO

    SHUKURANI

    Kwanza kabisa napenda KUMSHUKURU MWENYEZI MUNGU kwa ulinzi na Baraka zake ulioniwezesha kukamilisha kazi hii ya tunu. Ninamshukuru kwa kunijalia afya njema kipindi chote nilipokuwa naandika kitabu hiki. 

    Wapo watu ambao lazima niwataje kutokana na msaada wao walionipatia. Napenda kutoa shukrani za pekee kwa Saidi Makelele aliyewahi kuwa mwanamuziki aliyeshiriki katika bendi za Super Volcano, Les Volcano, Magola International, Jobiso, Les Wanyika, Simba Wanyika, Super Wanyika, Les Cuban (Vina Vina) na bendi zingine akipiga chombo cha tarumbeta, Kibwana Magati aliyekuwa mpiga ngoma (drums) katika bendi ya Morogoro jazz, Super Volcano, Les Wanyika pia David Senyagwa aliyekuwa anapiga gitaa la kati Cuban Marimba na Super Volcano, Robert Simba aliyekuwa mtunzi na mwimbaji Cuban Marimba, Super Volcano na Mzinga troupe na Muhtaji Mbaraka mtoto wa Mbaraka Mwinshehe anayeendeleza kazi ya baba yake kwa utayari wao kushirikiana nami katika kutoa taarifa muhimu na za kina, zilizochangia kukamilisha kitabu hiki. Bila ushirikiano huo, taarifa hizo muhimu juu ya harakati za muziki za gwiji Mbaraka Mwinshehe Mwaruka na mchango wake katika muziki wa rumba nisingeweza kuzipata kikamilifu.

    Pia nachukua nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa wanamuziki wote waliokubali ombi langu la kurudia baadhi ya kazi za nguli huyu pia kwa kushiriki katika kazi hiyo. Ikiwa ni pamoja na Muhtaji Mbaraka Mwinshehe Mwaruka aliyepiga gita la besi na kuimba, Omari Seseme aliyepiga gitaa la solo na gitaa la kati na kuimba pia Saidi Makelele aliyepiga chombo cha tarumbeta bila kumsahau Jaydrama wa KC Records aliyerekodi nyimbo hizo, kupiga kinanda na kuchanganya muziki. Nyimbo hizo ni Morogoro yapendeza, Esta, Shida na Soniasa.

    .

    1 UTANGULIZI

    Mbaraka Mwinshehe Mwaruka ni moja ya wanamuziki nyota kuwahi kutokea Tanzania. Mwanamuziki huyu alikuwa na kipaji kikubwa cha kupiga gitaa la solo, ala zingine, kutunga na kuimba. Kutokana na utunzi wake wa nyimbo za kusisimua, alijizolea wapenzi wengi wa muziki Afrika Mashariki na ya kati, akipiga zaidi muziki wa mtindo wa rumba, mtindo ambao asili yake ni kutoka Cuba na nchi zingine za Marekani ya kusini. Katika uhai wake, alishiriki kupiga muziki katika bendi za Morogoro jazz na Super Volcano zote za mjini Morogoro. Kitabu hiki Kinaanza kwa kuelezea kuingia kwa muziki wa rumba toka Cuba wakati huo Tanganyika na kuenea kwake, kinajikita zaidi kuelezea mchango wa mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe Mwaruka, katika kuundeleza na kuimarisha muziki huu wa rumba, kama sehemu ya juhudi za kuinua utamaduni wa taifa jipya la Tanzania na changamoto alizopitia.

    Muziki ni aina ya sanaa inayotumia sauti za binadam na ala za muziki ama kwa pamoja ama kila kimoja peke yake kwa mpangilio maalum. Muziki unapotiririka kutoka kwa wapigaji ama waimbaji kwenda kwa wasilikizaji ama wahusika, huibua hisia ama kuburudisha moyo. Kwa jinsi hii muziki hutungwa, kutafsiriwa na hata kuchezwa. Kwa jamii nyingi za kiafrika, muziki kama sehemu ya utamaduni wa jamii, ni kielelezo cha maisha ya binadamu na mahusiano yake na wenzake, iwe ni katika sherehe ya kuzaliwa, mavuno, tambiko, tiba, sherehe za ndoa, misiba na matukio mengineyo mbalimbali, kiasi kwamba, ni vigumu kufikiria maisha bila muziki. Hii ina maana kwamba muziki kama sehemu ya utamaduni wa jamii za kiafrika, unabeba maana pana zaidi ya dhana ya kuburudisha. Ndio maana, neno muziki kama burudani tu kwa jamii za kiafrika ni dhana ngeni, jina linalotumika zaidi ni ngoma kuelezea matukio hayo ya kijamii. Kwa hiyo, kuna ngoma ya mavuno, ngoma ya tiba na hata ngoma hizo hupewa majina maalum, madogori kwa mfano, ni ngoma ya tiba kwa wazaramo na waluguru.

    Kwa hiyo muziki ni sehemu ya mfumo wa pamoja wa jamii kimaisha, vipengee vingine vya mfumo huo vikiwa lugha, sanaa, imani, michezo, ujuzi, maadili, desturi, tabia, na kazi zingine za sanaa ambazo kwa pamoja hutambulika kama utamaduni na hutumika na wanajamii husika, kukabiliana na changamoto za dunia na mahusiano baina yao. Utamaduni huu, japo hurithishwa toka kizazi hadi kizazi, hubadilika kutokana na kukua kwa teknolojia, kuibuka kwa maarifa mapya shughuli za kisiasa, kijamii na kiuchumi. Kwa kutambua umuhimu wa utamaduni, mwaka 1962 mara baada ya Tanganyika kuwa jamhuri serikali mpya iliunda wizara ya utamaduni wa taifa na vijana. Nguzo za utamaduni zilizoainishwa ni pamoja na lugha, mila, desturi, sanaa na michezo, historia yetu, vielelezo vya utamaduni na utunzaji wa mazingira. Kwa kutambua hilo, sera hii ya utamaduni ililenga kujenga na kudumisha utambulisho huu wa taifa kwa njia ya kuendeleza maadili, mila na desturi nzuri na kuinua lugha ya Kiswahili kama chombo cha mawasiliano.

    Jambo linalochangia sana katika kukua kwa utamaduni, ni maingiliano kati ya jamii na jamii nyingine. Maingiliano hayo ni ya kawaida na husababisha jamii moja kupokea baadhi ya mambo ambayo ni mageni kwao. Lakini kwa kawaida jamii inayopokea mambo hayo mapya: kwanza huyachuja, kisha huyapa sura, vionjo, mwelekeo wa kisheria, kanuni, tabia na maadili ya jamii husika na kuyafanya kuwa yao. Mapokezi ya taratibu za maisha ya jamii nyingine na kuyaingiza katika jamii nyingine moja kwa moja, ni kuiga kama kasuku. Mapema kabisa serikali mpya ya kitaifa ya Tanzania iligundua kwamba, jambo la kupokea ama kuiga taratibu za maisha ya jamii nyingine likiachiwa hivihivi, litaathiri utamaduni wa asili wa jamii mzima na kuifanya kuwa kama mtumwa wa jamii yenye utamaduni ulioigwa.

    Moja ya mapokeo hayo, ni muziki wa dansi, ulioingia katika sehemu hizi za Afrika katika miaka ya 1930, na hasa mara baada ya kwisha kwa vita vya pili vya dunia. Muziki huu, ukakubalika na kuenea kwa kasi sehemu kubwa ya Afrika mashariki na ya kati. Kama ilivyokwisha elezwa, jambo hili ni la kawaida kwa kuwa moja ya jambo linalofanya utamaduni kukua ni maingiliano ya watu na mapokezi ya vitu vipya katika jamii. Lakini swali, ni je? mapokeo ya muziki wa dansi ama rumba yamezingatia taratibu za mapokezi ya kitu kigeni katika utamaduni wa jamii nyingine ama la. Kitabu hiki kinajaribu kujibu swali hili kwa kuelezea safari ya mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe Mwaruka ambaye ni mmoja wa wanamuziki bora kuwahi kutokea nchini ambaye kama wanamuziki wengine wa wakati huo naye aliupokea muziki huu wa rumba na kushiriki kuundeleza kwa njia ya tungo, kuupiga katika kumbi na hata kurekodi na kuuza nyimbo hizo. Mwanamuziki huyu kama mwenyewe anavyojieleza alitoa ahadi ya kukuza na kuendeleza utamaduni wa Mtanzania. Mbaraka anatoa ahadi ya kufanya hivyo katika wimbo alioutunga na kuimba akiwa na bendi yake ya Super Volcano. Kamwe sitakata tamaa kuendeleza utamaduni Tanzania, ...Utamaduni ndio roho ya taifa Volcano itadumisha kwa nguvu moja masika hoyee. Je ni kweli alifanya hivyo.

    Katika kujibu swali hili kitabu kinaanza kwa kutoa historia ya kuingia kwa muziki wa kigeni, hususani muziki wa rumba katika eneo hili la Afrika na kuenea kwake. Pili kinaelezea mchango wa mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe Mwaruka katika kuukuza muziki huu kwa lengo la kuutambulisha kama sehemu ya utamaduni wa Mtanzania, na changamoto alizopitia. Mwisho kinagusia suala la kuinua na kuendeleza muziki wa rumba kama harakati za kubuni mdundo wa muziki wa kitambulisho cha taifa.

    Kama inavyoonyeshwa katika kitabu hiki kazi hii ya kuingiza muziki wa rumba katika utamaduni wa Mtanzania iliishaanza bali haijakamilika. Kitabu kinahitimisha kwa kudai kwamba kwa kuwa muziki wa rumba ama wa dansi, ulikwisha onyesha njia kuelekea kubuni mdundo wa taifa basi upewe nafasi zaidi.

    2 HISTORIA YA MUZIKI WA DANSI TANZANIA

    Muziki wa awali kuingia nchini enzi za ukoloni, uliotangulia muziki wa dansi, ulijulikana kama muziki wa beni. Muziki huu unafanana na ule wa brass band za jeshi na za polisi. Watu wa kwanza kuvutika na aina hii ya muziki, ni wanajeshi na polisi kutoka katika jamii mbalimbali barani Afrika waliojiunga na jeshi la kikoloni, hasa wale waliojiunga na jeshi lililopigana katika vita vya pili vya dunia. Mapenzi ya muziki huu, yalijengeka miongoni mwa wanajeshi kwa kuwa ndio waliokuwa wakiusikia mara kwa mara, wakati ukitumika katika kwata na sherehe za kijeshi. Wale waliovutika sana na muziki huu, walijitahidi kuuendeleza hata baada ya vita kuisha na baada ya kustaafu jeshi. Lakini waliuendeleza kwa namna nyingine kabisa, kwanza waliupa vionjo vya kiafrika na hata ukatokea kupata wapenzi wengi sana ambao sio waliukubali tu bali pia waliuendeleza, kiasi kwamba ukakua na hata kutambulika zaidi kama muziki wa kiafrika.

    Ngoma ya mganda ya jamii za mkoa wa Ruvuma ni mojawapo ya muziki wa namna hii. Washiriki wake wakivaa nguo zinazofanana kama wanavyovaa askari: ila wao walifanya ubunifu mwingine badala ya sare za kijeshi walivaa shati jeupe, kaptula nyeupe na wakati mwingine hata tai, soksi ndefu nyeupe na

    Enjoying the preview?
    Page 1 of 1